Historia ya manispaa ya Furth

Manispaa ya Furth

Historia ya manispaa ya Fürth Manispaa ya Fürth Manisapaa ya Furth ina historia ya kabla ya Ukristo: Wakati wa kazi ya ujenzi kwenye eneo jipya la makaburi mnamo mwaka wa 1984, mabaki ya makaazi ya maisha ya ufinyanzi kutoka takriban miaka 4,500 kabla ya kuzaliwa Yesu Kristo (KK) na mabaki ya utamaduni wa Münchshöfen takriban 3,000 KK yalipatikana. Jina la eneo hilo limetokana na barabara ya zamani ivukayo bonde pana na iliyowekwa wakati ambapo Watawala wa Ebersberg walitaka kutengeneza muunganisho wa usafiri kati ya tawala zao mbili, Tondorf na Pfeffenhausen.

Mahala hapa pametajwa kwa mara ya kwanza katika waraka wa kichwa cha „Marktwart de Furte“ ambao unaonyesha mchango wa shamba ulitolewa kwa nyumba ya watawa ya Ebersberg karibu mwaka wa 1030.

Mnamo mwaka wa 1972 parokia ya Schatzhofen ilijiunga na Furth na tangu wakati huo muhuri wa parokia hiyo unajumuisha upanga wa mtakatifu Michael wa kanisa hilo. Kama mojawapo ya parokia kongwe zaidi katika wilaya hiyo, ilianzishwa katika karne ya nane.

Katika mwaka wa 1978, kama sehemu ya mageuzi ya mipaka, Arth pia ilijumuishwa katika wilaya ya Furth. Eneo hili lina historia ndefu sana. Nyaraka za michango kutoka miaka ya 814 na 822 zinaonesha umiliki wa ardhi katika eneo hili. Arth ilitajwa kwa mara ya kwanza katika nyaraka hizi mnamo mwaka wa 1028. Katika Nembo ya Furth, gurudumu lililovunjika la mtakatifu Catherine linasimamia jumuiya ya zamani.

Furth imekuwa na nembo mpya tangu mwaka 2001: katika rangi ya fedha, upau mwekundu wa ulalo uliofunikwa na upanga wa dhahabu (hii inamwakilisha mtakatifu Michael, mlinzi wa kanisa la Schatzhofen); juu yake ni picha ya dubu mweusi, anayetembea (ambaye anatokana na nembo ya familia ya kifahari ya Kärgl), chini yake ni gurudumu jeusi la Catharine linalojitokeza kwenye upauwa ulalo (Mtakatifu Catharine ndiye mtakatifu mlinzi wa la Kanisa la Arther – hilo gurudumu lapitikana pia katika nembo ya zamani ya manispaa). Kama vile Kurugenzi Kuu ya Hifadhi ya Kumbukumbu ya jimbo la Bavaria ilivyosema, mchoro wa nembo mpya unatosheleza mahitaji ya kisanaa na ya kihubiri.

Manispaa ya Furth, ambayo pia ni makao makuu ya jumuiya ya tawala zenye jina moja za Weihmichl na Obersüßbach, iko katika eneo lenye mandhari mazuri sana. Bonde la Further na makanisa yake kadhaa pamoja na uhifadhi wa misitu na mambo ya kilimo yanaangazia mandhari tofauti. Mbali na wilaya za Furth, Arth, Schatzhofen na Edmannsberg, kuna idadi ya kadhaa ya vitongoji na mashamba makubwa ya watu binafsi. Maeneo mawili ya makaazi ya zamani, ambayo watu hukaa hasa kujipumzisha siku za mwisho wa wiki pia yameijuishwa katika mandhari yake. Idadi kubwa ya kazi za ufundi, huduma na biashara hukidhi mahitaji ya ndani na ya kikanda. Maduka kadhaa yanavutia kwa manunuzi. Nyumba tisa za kulala wageni, baadhi zao zikiwa na malazi ya usiku mmoja-zinahakikisha ubora na ustawi wa kimwili. Kuna hoteli moja ndogo inayotoa mazingira murwa ya mikutano na makongamano. Jumba jipya la ghorofa katika majengo ya zamani kwenye uwanja wa gofu hutoa mazingira mazuri sana za malazi. Vile vile kuna nafasi mbalimbali za matibabu mahali hapa.

Ikiwa na idadi ya zaidi ya wakaazi 3,000 mji huo mdogo wa Furth una miundombinu mizuri sana isiyo ya kawaida. Nyumba za kuwalea watoto, shule za kawaida, shirikishi na chechekea za msituni, kuwafuatilia watoto wakati wa chakula cha mchana, malezi ya baada ya shule jioni, kufuatilia kazi wanazopewa watoto kufanyia nyumbani, Shule za msingi na sekondari na shule ya sekondari ya Maristen, maktaba kubwa kuu mpya, kituo cha kujifunza na tiba, kituo cha ushauri nasaha kwa vijana na chuo kikuu cha Ludwig-Maximilian hutengeneza taswira ya kipekee kwa ukubwa wa jumuiya hiyo ndogo ya Bavaria. Kituo cha manispaa cha kutoa elimu kwa watu wazima huendeshwa na jamii jirani za Obersüßbach na Weihmilch. Nyumba ya watawa ya Marist ina umuhimu mkubwa kwa jamii hiyo kutokana na umaarufu wake na mawasiliano ya kitaifa. Idadi kubwa ya vyama huboresha maisha ya kijamii, huandaa matukio ya burudani na husaidia eneo hilo katika shughuli tofauti za kijamii. Katika ngome ya zamani ya Fürth, kuna makaazi ya wazee ya Caritas, ambayo huwawezesha wazee kuishi maisha bora baada ya kustaafu. Kwa wakati huu nyumba mpya za wazee inajengwa katikati mwa kijiji. Pamoja na kituo kipya cha kijiji, wazo jipya la kuzingatia mambo mazuri ya kiikolojia limetiliwa maanani sana. Katika manispaa ya Fürth, thamani imewekwa kwenye kudumisha na kuboresha misingi ya kiikolojia na kiuchumi, ili vizazi vijavyo pia viweze kuishi Fürth katika njia bora, kufanya manunuzi ya bidhaa, kufanya kazi, kujifunza mengi na kutumia muda wao wa burudani katika mambo mengi. Mbinu mpya za usambazaji nishati, mpango mpana wa maeneo na vyanzo vya maji, umakini wa maendeleo ya ndani, matumizi ya rasilimali kwa mahitaji ya ndani, muundo wa kirafiki wa mazingara ya ardhi ya ujenzi pamoja na makaazi ya biashara na pia kuendeleza fursa Zaidi za burudani vinakusudia kuongeza ubora wa maisha. Mpango wa „Ugavi wa ndani ni ubora wa Maisha” huimarisha miundombinu na una nia ya kuongeza ufahamu kwamba ni wakaazi wenyewe ndio wanaojibika kwa maendeleo ya makaazi yao na mahali wanakoishi. Shughuli mbali mbali za wakaazi na jamii pia zimetambuliwa nje ya Furth. Kwa mfano, Furth ndio manispaa inayotumiwa kama mfano bora wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya kuhusu nishati jadidifu, jamii ya mfano kwa serikali ya jimbo la Bavaria katika mambo ya ugavi wa ndani na sekta ya nishati ambayo ni sehemu ya Ajenda ya 21 na pengine jamii ilyotuzwa mara nyingi Zaidi jimboni Bavaria kwa maendeleo uendelevu.